Na Hassan Abbasi:
WAKATI mwaka 2011 Rais
Jakaya Kikwete akiumiza kichwa kusaka majibu ya namna ya kuwa na mfumo
utakaosukuma mageuzi katika sekta za kiuchumi na kimajii, huenda hakuwa na
ufahamu wa madhila aliyokuwa nayo Mzee Nzowa.
Mzee Francis B. Nzowa wa
Msanyila, Mbozi, Mbeya ni kama wakulima wengine wengi nchini, amekuwa akilima
kwa bidii, akijitoa kuishi shamba lakini kilimo chake kilikuwa na changamoto
nyingi. Ni mambo kadhaa ya sadfa tu yakatokea na kubadili maisha yake.
Ni kama sadfa tu, nimesema
kwa sababu wakati Mzee Nzowa akihaha kusaka majibu ya namna ya kukifanya kilimo
chake kiwe cha tija n ahata wakati mwingine kukata tamaa, Rais Kikwete naye chini
ya maono makuu anaamua, baada ya kuona mafanikio ya nchini Malaysia, kuanzisha
BRN hapa nchini.
BRN ukiwa mfumo maalum na
wa kisayansi wa utekelezaji wa miradi kwa kuweka vipaumbele, kuibua mikakati ya
ufuatiliaji makini na ndani ya muda mfupi, unaanzishwa nchini Julai, 2013 na
kwa sadfa tu, sekta ya kilimo inaingizwa kuwa moja ya sekta za kipaumbele kati
ya nyingine sita.
Ni sadfa nyingine lakini
yenye faraja katika maisha ya Mzee Nzowa baada ya maeneo ya kipaumbele ndani ya
sekta ya kilimo nayo kuwa na moja ya malengo yake ni kujenga maghala na kuwasaidia
wakulima kupata masoko.
Katika mahojiano nami
jijini Dar es Salaam wiki iliyopita wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Mwaka wa
kwanza wa BRN, Mzee Nzowa anazungumza kwa hisia kali anapozikumbuka siku za
maisha yake kabla ya ujio wa mikakati ya BRN.
“Mimi ni mkulima wa
kahawa kama zao kuu la biashara na mahindi kama zao la chakula. Kwa kweli
tulijitahidi kulima lakini kuna maeneo ni kama tulikuwa kizani,” anaanza
kusimulia akiwa na hisia nzito na kuendelea:
“Hatukuwa na ufahamu wa
namna ya kukausha mazao, kuyatenga kwa madaraja bila kuchanganya mfano mahindi
na takataka nyingine ili kuweza kupata ubora na soko zuri.”
Anapokumbuka aina ya
uhifadhi wa zamani Mzee Nzowa anabadilika, uso wake katika wajihi mweusi
unakunjika na kutoa ishara ya kukumbuka jambo.
Nalibaini hilo kutokana
na uzoefu na uzeefu wangu katika kufanya mahojiano na watu mbalimbali kama
mwanahabari. Saikolojia ya unayemhoji ni muhimu zaidi katika kuendelea kupata
habari nzuri na usiyoitarajia.
Nasimama hapa na kuzidi kumdadisi
zaidi naye anafunguka: “Zamani tulikuwa tulipata hasara sana. Aina ya uhifadhi
wetu wa mazao ulikuwa sio wa kitaalamu.
“Mwaka 2011 nilipoteza
magunia 30 kati ya 60 ya mahindi niliyokuwa nimeyahifadhi kutokana na kushindwa
kuwa na utaalamu wa uhifadhi na kukosa soko,” anakumbuka na kuongeza:
“Mbaya zaidi mwaka uliofuata
magunia yangu yote 60 yaliharibika na nililazimika kulisha wanyama baada ya kukosa
mbinu bora za uhifadhi na sisi wakulima kuuziwa dawa feki tuliyodanganywa kuwa
ingelinda mazao yetu.”
Ujio wa BRN
Katikati ya madhila haya
yote na jakamoyo alilokuwa nalo Mzee Nzowa, vijana wa BRN, wataalamu wa kilimo
waliopewa hamasa na ari ya kuhakikisha tunakigeuza kilimo kuwa na tija zaidi na
manufaa kwa wakulima wakafika katika wilaya ya Mbozi.
Na kwa sadfa tena, vijana
wa BRN wakafika katika eneo la Mzee Nzowa na ananikumbusha mageuzi aliyofanyiwa
akisema. “Tulianza kupitia vyama vyetu vya ushirika kupewa mafunzo juu ya
matumizi ya mbegu bora za mahindi, kuvuna, kukausha na namna ya kuhakikisha
mazao yetu yanapangwa kwa ubora kwa kutochanganya na vitu vingine.
“Tulipewa kifaa cha
kupima unyevu katika mazao ili kujua uendelee kuyakausha au la. Na zaidi
tumejengewa maghala 30 ya kuhifadhi kisasa mazao na kutafutiwa masoko. Tulikuwa
tunakosea na kuondoa ubora wa chakula kwa kumwagilia dawa katika mahindi
yenyewe.
“Sasa hivi wataalamu
wametuelekeza wapi pa kupata dawa halisi ya kuhifadhi mazao isiyo feki na
kwamba tunapaswa kumwaga dawa eneo la ghala kabla ya kuweka mazao na kisha
kumwaga dawa nje ya ghala mara kwa mara kuzuia wadudu kuingia ghalani.”
Baada ya mageuzi haya ya
kilimo kupitia mikakati ya BRN, Mzee Nzowa akiwa na uso wa tabasamu ambalo
nililikosa kwa sehemu kubwa ya mahojiano yetu anasema: “Mafunzo na ushauri
tulioupata umeniongezea hamasa ya kulima zaidi. Kwangu sasa mahindi si zao la
chakula tu bali la biashara ninaloanza kulitegemea.
“Msimu wa mwaka jana
ambao ndio haya mazao tuliyonayo sasa nimevuna kuliko wakati wowote. Nimevuna
magunia 140! Nimeuza magunia 100 kwa wakala wa Serikali na sasa ninayo magunia yangu
40 kwa ajili yangu mwenyewe na yako salama hayajaharibika.”
Nilipogundua kuongezeka
kwa tabasamu la Mzee Nzowa nikampa nafasi zaidi kujieleza. “Hata bei tuliyopata
hivi sasa ni nzuri tofauti na kabla ya BRN. Nilikuwa nauza debe la mahindi kwa
kati ya Sh. 2,000 na 3,000. Mwaka huu yale magunia 100 nimeuza kilo Sh. 500 kwa
debe na kama unavyojua debe lina kilo 18 na gunia lina kilo 100. Fedha hii
sijawahi kuipata.”
Mwisho wa mahojiano Mzee
Nzowa ananiambia hana la kusema zaidi ya kushukuru waliokuja na wazo hili la
BRN na ananiahidi: “Tuonane mwakani nitakuonyesha zaidi mafanikio yangu, huu
ulikuwa mwanzo tu na hata fedha za mahindi niliyouza ndio nimeambiwa zimeingia
sasa kwenye akaunti. Nitakuwa mtu tofauti kabisa nikirudi MBozi,” anahitimisha
na kuniachia tabasamu.
Maisha ya Mzee Nzowa ni
matokeo yanayoonekana ya ubunifu na utekelezaji katika mpango wa BRN. Ni maisha
yanayoonesha matokeo ya watu kutafakari na kutafuta majibu ya changamoto
tulizonazo.
*Makala haya yamechapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Mwananchi, Machi 12, 2015.