Nyumbani / Habari / Miradi / Mawasiliano

Ubunifu BRN-kilimo wabadili maisha ya Mzee Nzowa

Leave a Comment

Na Hassan Abbasi:

WAKATI mwaka 2011 Rais Jakaya Kikwete akiumiza kichwa kusaka majibu ya namna ya kuwa na mfumo utakaosukuma mageuzi katika sekta za kiuchumi na kimajii, huenda hakuwa na ufahamu wa madhila aliyokuwa nayo Mzee Nzowa.

Mzee Francis B. Nzowa wa Msanyila, Mbozi, Mbeya ni kama wakulima wengine wengi nchini, amekuwa akilima kwa bidii, akijitoa kuishi shamba lakini kilimo chake kilikuwa na changamoto nyingi. Ni mambo kadhaa ya sadfa tu yakatokea na kubadili maisha yake.

Ni kama sadfa tu, nimesema kwa sababu wakati Mzee Nzowa akihaha kusaka majibu ya namna ya kukifanya kilimo chake kiwe cha tija n ahata wakati mwingine kukata tamaa, Rais Kikwete naye chini ya maono makuu anaamua, baada ya kuona mafanikio ya nchini Malaysia, kuanzisha BRN hapa nchini.

BRN ukiwa mfumo maalum na wa kisayansi wa utekelezaji wa miradi kwa kuweka vipaumbele, kuibua mikakati ya ufuatiliaji makini na ndani ya muda mfupi, unaanzishwa nchini Julai, 2013 na kwa sadfa tu, sekta ya kilimo inaingizwa kuwa moja ya sekta za kipaumbele kati ya nyingine sita.

Ni sadfa nyingine lakini yenye faraja katika maisha ya Mzee Nzowa baada ya maeneo ya kipaumbele ndani ya sekta ya kilimo nayo kuwa na moja ya malengo yake ni kujenga maghala na kuwasaidia wakulima kupata masoko.

Katika mahojiano nami jijini Dar es Salaam wiki iliyopita wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Mwaka wa kwanza wa BRN, Mzee Nzowa anazungumza kwa hisia kali anapozikumbuka siku za maisha yake kabla ya ujio wa mikakati ya BRN.

“Mimi ni mkulima wa kahawa kama zao kuu la biashara na mahindi kama zao la chakula. Kwa kweli tulijitahidi kulima lakini kuna maeneo ni kama tulikuwa kizani,” anaanza kusimulia akiwa na hisia nzito na kuendelea:
 

“Hatukuwa na ufahamu wa namna ya kukausha mazao, kuyatenga kwa madaraja bila kuchanganya mfano mahindi na takataka nyingine ili kuweza kupata ubora na soko zuri.”

Anapokumbuka aina ya uhifadhi wa zamani Mzee Nzowa anabadilika, uso wake katika wajihi mweusi unakunjika na kutoa ishara ya kukumbuka jambo.

Nalibaini hilo kutokana na uzoefu na uzeefu wangu katika kufanya mahojiano na watu mbalimbali kama mwanahabari. Saikolojia ya unayemhoji ni muhimu zaidi katika kuendelea kupata habari nzuri na usiyoitarajia.

Nasimama hapa na kuzidi kumdadisi zaidi naye anafunguka: “Zamani tulikuwa tulipata hasara sana. Aina ya uhifadhi wetu wa mazao ulikuwa sio wa kitaalamu.

“Mwaka 2011 nilipoteza magunia 30 kati ya 60 ya mahindi niliyokuwa nimeyahifadhi kutokana na kushindwa kuwa na utaalamu wa uhifadhi na kukosa soko,” anakumbuka na kuongeza:

“Mbaya zaidi mwaka uliofuata magunia yangu yote 60 yaliharibika na nililazimika kulisha wanyama baada ya kukosa mbinu bora za uhifadhi na sisi wakulima kuuziwa dawa feki tuliyodanganywa kuwa ingelinda mazao yetu.”

                                                Ujio wa BRN

Katikati ya madhila haya yote na jakamoyo alilokuwa nalo Mzee Nzowa, vijana wa BRN, wataalamu wa kilimo waliopewa hamasa na ari ya kuhakikisha tunakigeuza kilimo kuwa na tija zaidi na manufaa kwa wakulima wakafika katika wilaya ya Mbozi.

Na kwa sadfa tena, vijana wa BRN wakafika katika eneo la Mzee Nzowa na ananikumbusha mageuzi aliyofanyiwa akisema. “Tulianza kupitia vyama vyetu vya ushirika kupewa mafunzo juu ya matumizi ya mbegu bora za mahindi, kuvuna, kukausha na namna ya kuhakikisha mazao yetu yanapangwa kwa ubora kwa kutochanganya na vitu vingine.

“Tulipewa kifaa cha kupima unyevu katika mazao ili kujua uendelee kuyakausha au la. Na zaidi tumejengewa maghala 30 ya kuhifadhi kisasa mazao na kutafutiwa masoko. Tulikuwa tunakosea na kuondoa ubora wa chakula kwa kumwagilia dawa katika mahindi yenyewe.

“Sasa hivi wataalamu wametuelekeza wapi pa kupata dawa halisi ya kuhifadhi mazao isiyo feki na kwamba tunapaswa kumwaga dawa eneo la ghala kabla ya kuweka mazao na kisha kumwaga dawa nje ya ghala mara kwa mara kuzuia wadudu kuingia ghalani.”

Baada ya mageuzi haya ya kilimo kupitia mikakati ya BRN, Mzee Nzowa akiwa na uso wa tabasamu ambalo nililikosa kwa sehemu kubwa ya mahojiano yetu anasema: “Mafunzo na ushauri tulioupata umeniongezea hamasa ya kulima zaidi. Kwangu sasa mahindi si zao la chakula tu bali la biashara ninaloanza kulitegemea.

“Msimu wa mwaka jana ambao ndio haya mazao tuliyonayo sasa nimevuna kuliko wakati wowote. Nimevuna magunia 140! Nimeuza magunia 100 kwa wakala wa Serikali na sasa ninayo magunia yangu 40 kwa ajili yangu mwenyewe na yako salama hayajaharibika.”

Nilipogundua kuongezeka kwa tabasamu la Mzee Nzowa nikampa nafasi zaidi kujieleza. “Hata bei tuliyopata hivi sasa ni nzuri tofauti na kabla ya BRN. Nilikuwa nauza debe la mahindi kwa kati ya Sh. 2,000 na 3,000. Mwaka huu yale magunia 100 nimeuza kilo Sh. 500 kwa debe na kama unavyojua debe lina kilo 18 na gunia lina kilo 100. Fedha hii sijawahi kuipata.”

Mwisho wa mahojiano Mzee Nzowa ananiambia hana la kusema zaidi ya kushukuru waliokuja na wazo hili la BRN na ananiahidi: “Tuonane mwakani nitakuonyesha zaidi mafanikio yangu, huu ulikuwa mwanzo tu na hata fedha za mahindi niliyouza ndio nimeambiwa zimeingia sasa kwenye akaunti. Nitakuwa mtu tofauti kabisa nikirudi MBozi,” anahitimisha na kuniachia tabasamu.

 

 
Maisha ya Mzee Nzowa ni matokeo yanayoonekana ya ubunifu na utekelezaji katika mpango wa BRN. Ni maisha yanayoonesha matokeo ya watu kutafakari na kutafuta majibu ya changamoto tulizonazo.
*Makala haya yamechapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Mwananchi, Machi 12, 2015.
Previous PostOlder Post Home

0 comments:

Post a Comment