Ujumbe wa Rais wa Ujerumani ulioko nchini
kwa ziara ya siku tano umeonesha kushangazwa na ubunifu ambao Serikali ya
Tanzania imeuanzisha katika utekelezaji wa miradi kupitia mfumo wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN).
Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam juzi
na Waziri wa Uchumi na Nishati wa Ujerumani, Bw. Matthias Machnig wakati ujumbe
wa wafanyabiashara wa Ujerumani ulipokutana na Mtendaji Mkuu Ofisi ya
Rais-Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB) inayosimamia BRN, Bw. Omari
Issa.
“Ubunifu huu wa utekelezaji wa miradi
kupitia BRN ni jambo ambalo hata sisi tunatamani tungekuwa nalo nchini
Ujerumani,” alisema Bw. Machnig.
Katika mkutano huo wafanyabiashara hao wa
Ujerumani walionesha shauku ya kuwekeza katika miradi ya ubia ya BRN ili
kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha kuwa mageuzi makubwa hasa
katika sekta za nishati na uchukuzi yanafanikiwa kwa mujibu wa malengo ya BRN.
Akizungumzia kuhusu mfumo wa BRN, Bw. Issa
aliwaeleza wageni hao kuwa Serikali ya Tanzania iliamua kuanzisha mfumo huu ili
kuharakisha utekelezaji wa miradi muhimu ya kitaifa na kuwaletea wananchi
maendeleo ya haraka.
Alisisitiza kuwa mfumo wa BRN unaamini
katika kuweka vipaumbele na kisha kusimamia na kufuatilia utekelezaji wake kwa
kuondoa urasimu na mtindo wa kufanyakazi kwa mazoea.
“Nitawapa mfano wa sekta ya kilimo katika
BRN. Tunatekeleza mageuzi katika sekta ya kilimo lakini si katika kila kitu.
Tumeanza na mazao matatu tu ya mahindi, mpunga na miwa tena si nchi nzima bali
sehe,mu tu ya nchi ndiyo tumeanza nayo. Mafanikio yatakayopatikana kupitia
vipaumbele hivi yatapelekwa mikoa mingine,” alisema Bw. Issa.
Aliwakaribisha wawekezaji hao kushirikiana
na Serikali ya Tanzania kwani tayari nchi mbalimbali zimekwishaonesha nia na
zimeanza kufanya hivyo. “Treni ya mabadiliko imeanza safari ni juu ya kila
mmoja wetu kuwahi ili awe sehemu ya safari hii,” alisema Bw. Issa.
Kwa kuwa BRN inasimamia utekelezaji
unaofanywa na wizara na taasisi za Serikali wawekezaji hao waliahidi kukutana
na kufanya mazungumzo zaidi ili kufikia makubaliano na wizara na taasisi
zinazomiliki miradi hito na Bw. Omari aliahidi kuwa wakifikia makubaliano hayo
PDB itasaidia kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi.
0 comments:
Post a Comment