Nyumbani / Habari / Miradi / Mawasiliano

Mkakati wa BRN kutatua tatizo la umeme nchini

Leave a Comment

 
 
Na Kenneth Mutaonga* 

WIKI hii tunaanza kuichambua miradi ya sekta ya nishati katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN). Baada ya utanguliza kuhusu BRN na baadhi ya sekta za mpango huu, nimefurahi kupata fursa hii kuzungumza na watanzania wenzangu kuhusu mageuzi ninayofuatilia kwa kila siku katika kazi zangu nikiwa Meneja wa sekta ya Nishati katika BRN.
 

Makala zangu hizi zitakuwa ni mfululizo wa wiki tatu hivi kutegemeana pia na maoni au hoja zitakazotolewa na wasomaji. Mosi leo nitaanza kwa kutoa maelezo ya jumla kuhusu mikakati ya BRN katika sekta ya nishati na nini hasa tunataka watanzania watupime nacho baada ya miaka miwili au mitatu.
 

Makala ya pili ambayo ni wiki ijayo nitaainisha mafanikio ambayo tumeyapata katika malengo tuliyoweka mpaka sasa. Tatu nitahitimisha kwa kujibu maswali ya wasomaji wetu au kama hakutakuwa na hoja nitatoa uzoefu wangu zaidi kuhusu manmbo yanayotokea katika sekta ya nishati na BRN na watanzania watarajie nini.

 
Kwa utangulizi tu niseme sekta ya nishati nchini inafahamika kwa kukumbwa na changamoto ya uhaba wa uzalishaji wa nishati ya umeme. Hali hii imesababisha mgawo wa mara kwa mara wa umeme na hata kuathiri maendeleo ya viwanda hapa nchini.
 

Kama ilivyoelezwa awali katika makala hizi, mfumo wa BRN ili kutatua kero zilizoainishwa huwaweka pamoja wadau katika maabara ambapo hukaa kwa takribani wiki sita kuchambua na kutoa suluhisho linalohusu sekta fulani.
 

Kwa minajili hiyo hiyo maabara ya sekta ya nishati, kwa kutambua changamoto zinazoigusa sekta hii, ilipendekeza imependekeza mambo mbalimbali kama malengo ya kisekta ambayo jamii itaalikwa kufuatilia utekelezaji wake na kutupima kwayo. Baadhi ya malengo yaliyowekwa ni:-


Mosi, kuongeza ufanisi wa uzalishaji na usambaziji umeme kutoka miradi iliyopo sasa. Mkakati huu unahusisha ukarabati, uendelezaji na ujenzi wa mitambo ya kuzalisha na kusambaza umeme katika sehemu mbalimbali nchini na hatua za kuboresha mabwawa ya kuzalisha umme wa maji. 

Pili, Kuongeza kiwango cha uzalishaji wa umeme kwa zaidi ya megawati 1300 mpya ili kuongeza katika gridi ya sasa ya Taifa. Lengo hili linaweza kutimizwa kupitia uzalishaji wa umeme wa gesi katika miradi minne inayoandaliwa ujenzi wake kwenye eneo la Kinyerezi Dar es Salaam na miadi mingine midogo midogo iliyoko sehemu mbalimbali nchini.
 

Tatu, Kuimarisha zaidi ya kilometa 3,000 za usambazaji wa umeme mkubwa. Katika hili ipo miradi saba ya kuboresha njia za usafirishaji wa umeme. Lengo ni kuhakikisha kuwa tunapunguza upotevu wa umeme lakini pia umeme unawafikia watumiaji kwa uhakika zaidi.
 
 

Nne, Kuwaunganisha wananchi laki 5 zaidi katika umeme wa gridi. Hii itatokana zaidi na kuimarika kwa uzalishaji kama nilivyoainisha hapo awali na hasa kupitia miradi ya usambazasi umeme vijijini chini ya REA.
 

Tano, kuondokana na mfumo wa kutegemea mitambo ya uzalishaji umeme wa dharura. Mitambo ya dharura inafahamika kwa gharama kubwa za uendeshaji. Katika mkakati huu wa BRN sekta ya nishati vyanzo nilivyobainisha mwanzo vya nishati kama vile gesi tunaamini vinaweza kusaidia nchi kuwa na umeme wa kutosha na hivyo kutohitaji mitambo ya umeme wa dharura.
 

Sita, Mageuzi katika sekta ya nishati ni mkakati mwingine muhimu ambao BRN inausimamia. Katika eneo hili lengo kuu ni kulifanya Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (Tanesco) kujiendesha kwa ufanisi zaidi kwa kuligawa shirika hilo kulingana na mahitaji ya jamii.
 

Ili kutekeleza mageuzi hayo tuliweka lengo la kuchapisha kitabu kinachoainisha mageuzi ya sekta ya nishati na pia Wizara kuwekewa lengo la kuja na sera ya kuiainisha namna mbadala ya kutoa ruzuku katika sekta hii. Yote haya yanalenga kuleta ufanisi.
 

                                                   Mfumo wa Utekelezaji
 

Katika Makala za awali kuhusu BRN mwenzangu Bw. Hassan Abbas amekuwa akisisitiza sana BRN kuwa na mfumo wa kipekee na nidhamu ya aina yake katikja utekelezaji wa miradi. Ili malengo ya sekta ya nishati yafanikiwe muundo wa utekelezaji wa malengo hayo umeshakamilika ambapo katika wizara ya nishati na madini tumeshaanzisha kitengo cha ufuatiliaji yaani Ministerial Delivery Unit (MDU).


Kitengo hiki kinahakikisha kuwa malengo niliyoyaainisha kila siku yanafikiwa kwa utekelezaji wa kasi kufanyika. Katika utekelezaji huo pale ambapo kuna suala linalohitaji wadau wa aina mbalimbali basi wote wanaitwa na kukaa pamoja ili kutatua changamoto.

 
Kwa mtindo huu wa utendaji, kama tutakavyoona wiki ijayo, matokeo makubwa yameanza kuonekana katika sekta ya nishati. Matokeo hayo, nitayazungumzia katika namna mabadiliko ya kifikra kiutendaji yalivyotokea lakini pia tutaangalia yale yanayohusu takwimu za utekelezaji wa miradi kwa mujibu wa malengo yaliyowekwa.


Tukutane wiki ijayo tutakapoanza kuangalia kwa kina mafanikio katika utekelezaji wa sekta hii chini ya miradi ya kipaumbele ya BRN.
 

*Mwandishi ni Meneja wa Sekta ya Nishati katika Ofisi ya Rais - Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi (PDB) inayosimamia utekelezaji wa BRN. Simu 0687 222 541; au baruapepe kmutaonga@pdb.go.tz

 
Next PostNewer Post Previous PostOlder Post Home

0 comments:

Post a Comment